Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatilia matangazo ya kazi sehemu mbalimbali Tanzania, lengo langu kubwa halikuwa kwa ajili ya kutafuta kazi, bali nilitaka kujua uelekeo wa ajira kwa nchi yetu ya Tanzania. Kwani, uelekeo huu ndio utakaoweza kubadirisha mustakabali wa ufanisi wa kazi na maendeleo kwa taifa letu.Pia, nilitaka kujua je waajiri wanajua nani wanayemtafuta?
Mwaka juzi nilipata nafasi ya kuwa mmoja msemaji mkuu (Key note speaker) katika mkutano wa kimataifa juu ya E Commerce na E Governance ulioandaliwa na IEEE hapa China, hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuwa katika uwanja kama ule mbele ya magwiji toka makampuni makubwa duniani. Katika mkutano ule, nilizungumzia kuhusu aina mpya ya biashara ya online kwa kutumia mitandao jamii (Social Commerce), ni mada iliyovuta hisia za watu wengi sana hivyo ilikaribisha maswali mengi mno.
Moja ya swali nililoulizwa na Mr Jen Yao Chung toka kitengo cha tafiti cha IBM Marekani( IBM T.J Watson Research Center) ni jinsi gani tutaweza kupima faida au mchango wa mitandao jamii(social networks) kwenye biashara za mitandaoni(ecomerce). Katika kumjibu swali lake, nilimuambia kuwa, tunatakiwa kuifanya mitandao jamii(social networks) kuwa sehemu ya biashara ili tuweze kupima na kuuchunga mchango wake.
Baada ya kuisha kwa mkutano ule, nilikuwa na mengi ya kubadirishana na Mr Chung, nilimuuliza kwanini uliamua kuuliza lile swali, alinijibu kwa kusema, kwa muda mrefu, kumekuwa na utofauti kati ya muono wa mamanager wa IT juu ya nini wanatakiwa kufanya na nini wanachokifanya. Wengi wao wanadhani wao ni kwa ajili ya kutoa huduma (outputs) badala ya matokeo (outcomes), na hii ndio sababu inafanya makampuni mengi kutoona faida za moja kwa moja za IT, pia IT kushindwa kusukuma gurudumu la maendeleo ya kampuni husika.Hivyo alinisihi kutumia muda mwingi kufahamu uelekeo sahihi wa IT toka ule wa zamani uliozoeleka. Haswaa kwa sisi nchi zinzoendelea.